Darasa toka kwa Millard Ayo wa Ayo TV

My Writings

Juzi Fulani nilikuwa mitaa ya Mwananyamala, Mala Paap! Nakutana na  Gari la AYO TV. Gari ambayo kwa namna moja ama nyingine ni gari yenye kuonesha mwelekeo wa huyu jamaa. Sikuwepo wakati Erick Shigongo anaijenga Empire yake au Mkurugenzi mtendaji wa IPP bwana Regnald Mengi alipo anza shughuri zake.

Nilikuwepo jana ambapo Bongo Records ndio ilikuwa Studio maarufu kwa hapa Tanzania ikipika na kupakua vipaji makini  katika muziki wa kizazi kilicho itwa kizazi kipya, wakisaidiana na studio na wadau kama kina Masta Jay.  Nipo leo ambayo Diamond Platnumz yupo Busy akiupeleka Muziki duniani, Akibadilisha maisha ya watu kadha wa kadha na kufanya vipaji kuwa ni kazi rasmi, akipambana kwa anavyo jua yeye na uongozi wake kuhakikisha Kila aina ya biashara wanayo ianzisha inakuwa na mafanikio kwa mapana yake.

Nipo Leo ambayo wanamuziki kama Ali Kiba wameona kuna umuhimu wa kujiongeza kadri wawezavyo na kuingia kwenye Biashara ya Vinywaji na kadhalika, Leo ambayo Msanii kama Niki Wa Pili ameamua kulikomboa taifa lake kupitia wazee na vijana wanao upenda muziki wake kwa kuwekeza katika elimu ili awe mfano wa kuigwa kwa walioko mashuleni natena wanatamani kutumia vipawa vyao katika Sanaa, wazazi na serikali kwa ujumla ijivunie kuwa na wanamuziki wenye elimu, adabu na Zaidi lugha na maneno yenye staha katika jamii.

Leo ambayo kila uchao Youtube inafulika video za kila aina na kwa mwenye kujifunza anatumia wakati na muda huo kujifunza kila aina ya elimu kwa gharama nafuu.

Lengo La Andiko Hili: Kuiona AYO TV ikiwa kazini Mwananyamala kulinifanya nitabasamu, na kukanipa muda wa kutafakari kwa kina na kujikuta nikitaka andika katika maandiko yangu ya #MpakaWakatiMwingine. Millard ni kijana mdogo kwa wenye uwezo wa kumuita hivyo,  Sina taarifa nzuri juu ya elimu yake Zaidi ya taarifa  ile niliyo nayo kutoka  mtaani yani redio zisizo rasmi ya kumaliza Form Four (Kidato Cha Nne) na matokeo yake kumkalia kushoto. Kwangu Millard Anawakilisha vijana wenye nia ya kufanikiwa iwe kwenye ajira au pasipo ajira. Ananikumbusha mbali na ananikumbusha wengi ninao wafahamu ambao kwa namna moja ama nyingine wamepambana na wanaendelea kupambana wakitumia watu kama Mengi, Shigongo, Kusaga na wadau wengine kama mifano.

Kumfuatilia kwangu YOUTUBE kumenifanya nijifunze kitu kwake, alikuwa na malengo kitambo, alijua anataka nini mapema na alitambua afanye nini na apite wapi, akaamua kutumia kila nyenzo aliyo iona inafaa ili aweze kufika alipo leo hii. Sina uhakika kama kuna stori nyingine nyuma ya pazia ila binafsi nimekoshwa na namna anavyo pambana kuhakikisha anatimiza malengo yake.

Sinto kuja shangaa nikisikia kesho AYO TV imekuwa ni Media kamili ikipatikana katika DSTV ama ZUKU. Zote ni ndoto na Zaidi ni kuzisimamia ndoto.

MUHIMU: Hakuna mtu au darasa litakalo kwambia tunaanza HIVI. Darasa muhimu na mtu muhimu ni wewe na nafsi yako, sahau urithi, sahau mali za baba na mama. Wewe ndiye mtu wa kwanza kuamua uishi vipi na ufanye vipi. Ajira uliyo nayo isiwe kikwazo au kigezo cha kutotimiza malengo yako.

Anasema “Vijana hawana budi kujitambua, watambue hakuna anaye fahamu au amini kirahisi Ndoto zako, hakuna anaye weza zielewa na kutamani timiza ndoto zako Zaidi yako, Mfano wake ni juu ya BANK Fulani kumnyima mkopo alio taka omba ili apanue wigo wa biashara yake.”

FUNZO: Endapo Millard ameweza nyimwa mkopo wa namna hiyo japo ni mtu mwenye kufahamika kila pande ya nchi hii, wewe je? Sijajua njia na namna alivyo i-approch bank husika ila ninajikuta nikiingiwa na hofu ikizingatiwa hakuna asiye mfahamu Millard Ayo na namna alivyo “potential”. Miaka kadhaa ijayo tunazungumzia Ka-Milionea Fulani amazing kutoka kwenye Sekta ya habari.

Kumbe hatuna budi KUKAZA hadi kieleweke pasipo kujali nani na kutoka wapi atasema nini, iwe ni ndugu, wazazi, familia au marafiki, cha msingi ni kusimamia ndoto zako pasipo kuvunja sharia na kanuni za dini yako pia nchi kwa ujumla, pia kuwa tofauti, mwenye hekima na busara.